Jumanne , 9th Aug , 2022

Kampuni ya michezo ya kubashiri mtandaoni ya Parimatch imetangaza kuingia makubaliano ya kuidhamini klabu ya Mbeya City kwa msimu wa 2022/23.

Makabidhiano ya jezi kama ishara ya udhamini wa kampuni ya Parimatch katika klabu ya Mbeya City

Hatua hiyo ni muendelezo wa udhamini wao kwa klabu hiyo kama ilivyofanya kwa msimu 2021/22, ambapo Afisa Habari wa kampuni hiyo Ismael Mohamed amesema wamefikia hatua hiyo kutokana na ukubwa wa Mbeya City na idadi ya mashabiki walionao.

"Mbeya City ni moja ya klabu kubwa kwa hapa Tanzania hususani ukiangalia idadi ya mashabiki na ushawishi katika soka na hiyo ndio sababu tosha ya sisi kurejea tena kufanya udhamini na Mbeya City kwa msimu huu mpya, kama mtakumbuka vizuri msimu wa 2020/2021 tulikuwa wadhamini wakuu kwa mara ya kwanza", amesema Ismail.

"Sisi kama Parimatch Moja ya jukumu letu kubwa ni kuhakikisha michezo inakua kuanzia ngazi ya chini hadi ngazi ya kimataifa. Lakini pia tunaendelea na michakato mablimbali ya kuunga mkono vilabu vingine kutoka ligi kuu,  ligi daraja la kwanza na hata Vilabu Chipukizi . Ikiwa ni kuunga mkono juhudi za TFF na bodi ya ligi kuhakikisha ligi za Tanzania zinakuwa na tunaenda Kimataifa", ameongeza.

Pamoja na kutoa pesa taslimu kwa timu hiyo, pia Parimatch pia itatoa vifaa kwa klabu pamoja na ukarabati mdogo wa uwanja wa Sokoine hasa katika eneo la kukaa la benchi la ufundi  kwa awamu.

Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa Mbeya City Emmanuel Kimbe amewashukuru kampuni ya Parimatch Tanzania kwa kusaini tena mkataba na timu hiyo huku kwa niaba ya klabu ya Mbeya City akiwaahidi klabu hiyo watatekeleza matakwa yote ya kimkataba yaliyopo kwenye mkataba huo.

Parimatch ni kampuni inayoendesha shughuli za michezo ya kubashiri mtandaoni ikiwa imesajiliwa na bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania kwa takriban miaka 5 sasa. Kimataifa ipo zaidi ya nchi 15 ikiwa na wateja zaidi ya milioni moja duniani kote.