Okwi atangaza mabadiliko

Tuesday , 5th Dec , 2017

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uganda na klabu ya Simba Emmanuel Okwi baada ya kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa ndani ametangaza kubadili jina analotumia kwenye mitandao ya kijamii.

Okwi ambaye jumamosi iliyopita ametangazwa kuwa mchezaji bora wa ndani ya Uganda wa msimu uliopita wa 2016/17, amebadili kwenye ukurasa wake wa Instagram kutoka lile la awali ambalo alikuwa anatumia (@emmosting) na sasa ametangaza kuanza kutumia jina lake la (@emmanuelokwi).

Jina hilo amelitangaza leo kupitia ukurasa wake huo wa Instagram akiwajulisha mashabiki wake ambapo ameendika, “Tafadhali pokeeni hii taarifa ya jina langu jipya nitakalokuwa natumia”.

Nyota huyo amekuwa kwenye kiwango kizuri tangu msimu uliopita aliporejea kwenye klabu yake iliyomlea na kukuza kipaji chake ya Sports Club Villa ya Uganda kabla ya kutua kwenye klabu ya Simba msimu huu.

Mganda huyo ndiye kinara wa mabao kwenye ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2017/18 baada ya raudni 11. Okwi ana mabao nane na anatarajiwa kurejea dimbani baada ya mapumziko mafupi ya ligi kupisha michuano ya CECAFA Challenge.