Jumamosi , 26th Mei , 2018

Baada ya sintofahamu ya muda mrefu juu ya hatima ya mchezaji wa kimataifa wa Yanga Donald Ngoma ndani ya klabu hiyo, hatimaye nyota huyo raia wa Zimbabwe amesajiliwa na klabu ya Azam FC.

Taarifa ya Azam FC imesema imeingia makubaliano na mshambuliaji huyo kwaajili ya msimu ujao wa 2018/19. Pamoja na kuthibitisha usajili huo, lakini uongozi wa wanalambalamba umegoma kuweka wazi mkataba baina ya pande
hizo mbili.

Msemaji wa Azam FC Jaffar Idd Maganga, ameenda mbali zaidi kwa kusema tayari mchezaji huyo ameandaliwa jezi namba 11 iliyokuwa ikitumiwa na mshambuliaji Yahaya Mohammed, aliyerejea Aduana Stars ya nchini kwao Ghana, baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na Azam.

Jaffar amesema baada ya makubaliano hayo na Ngoma, wanatarajia kumpeleka katika Hospitali ya Vincent Pallotti jijini Cape Town, Afrika Kusini kwa ajili ya kumfanyia vipimo vya afya ili kuona ni kwa kiasi gani majeraha yaliyokuwa yakimsumbua yamepona au kama anahitaji matibabu zaidi.

Ngoma alijiunga na Yanga msimu wa 2016/17 akitokea FC Platinum ya Zimbabwe, na alitoa mchango mkubwa kwa Yanga msimu huo, ikifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na kubeba mataji mawili, Ligi Kuu na Kombe la FA.

Msimu huu unaomalizika Jumatatu ya Mei 28, Ngoma hajawa sehemu ya kikosi cha Yanga, kutokana na kuwa majeruhi kwa muda mrefu ambapo ilifika muda uongozi ukataka kumuondoa. Awali, Ngoma alikuwa na mkataba wa miaka miwili kabla ya mwaka jana kuripotiwa kuongeza tena miwili.