Jumatano , 15th Feb , 2017

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye amewataka wananchi waliojenga maeneo ya wazi yaliyotengwa kwa ajili ya Viwanja vya Michezo kuhakikisha wanayaachia ili yaweze kutumika kama ilivyopangwa.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (aliyesimama mbele) akiongea na Wageni waalikwa pamoja na Waandishi wa habari wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa kiwanja cha Baseball nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Japan leo 15 Februari, 2017 Jijini Dar es Salaam.

 

Mhe. Nape amesema, wameshaandaa Program maalum ambayo itahusika na kufuatilia watu waliyojenga maeneo ya wazi ambayo yametengwa maalum kwa ajili ya viwanja vya Michezo ili kuhakikisha kunakuwa na viwanja vingi ambavyo vitawasaidia watoto kuweza kupata maeneo ya kuendeleza vipaji vyao.

"Tumeweka Programu maalum kwa ajili ya kufuatilia na kuhakikisha waliovamia maeneo ya wazi ambayo yaliwekwa kwa ajili ya viwanja vya michezo yanarudishwa na kutumiwa kama ilivyopangwa na hakutakuwa na mbadala kwa sababu wapo watu wamejenga katika maeneo hayo na wakiambiwa waondoke wanataka fidia," amesema Nape.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye akiwa katika picha ya pamoja na Wachezaji wa mchezo wa Baseball mara baada ya hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa kiwanja cha Baseball nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Japan leo 15 Februari, 2017 Jijini Dar es Salaam.

Nape amesema, anaamini maeneo ya wazi yaliyovamiwa yapo mengi na jitihada za kuyarudisha zitafanyika kama ilivyoahidiwa ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na maeneo ya karibu ya kufanyia mazoezi na hata watoto pia wanapata viwanja kwa ajili ya michezo.

Wakati huohuo Nape amesema, kwasasa serikali kwa kushirikiana na wadau wa michezo nchini inajipanga kuhakikisha ushiriki wa wanamichezo wa Tanzania katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2020 nchini Japan unaongezeka ili kuongeza uwezekano wa kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Mwenyekiti wa Chama cha Baseball Tanzania (TaBSA), Dkt. Ahmed Makata (aliyekaa kushoto mbele) akisaini Mkataba wa Ujenzi wa Uwanja wa Baseball, kulia ni Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mhe. Masaharu Yoshida.Wanaoshuhudia nyuma ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye pamoja na Mjumbe toka Japan.