Jumatatu , 15th Feb , 2021

Mshambuliaji mahiri wa Arsenal Pierre Americk Aubameyang,  jana alifuga magoli matatu 'hattrick' katika mchezo dhidi ya Leeds United, uliomalizika kwa Arsenal kupata ushindi wa bao  4-2.

Nahodha wa Arsenal Pierre Americk Aubameyang

Ilikuwa siku nzuri kwa Aubameyang kwa kuanza kufunga goli mapema katika dakika ya 13 na kisha kuongeza mengine katika dakika ya  41 na 47 kabla ya Hector Bellerin, kufunga dakika ya 45  na kumaliza  mechi hiyo  kwa 'hattrick' yake ya kwanza tangu achaguliwe kuwa nahodha na pia ni 'hattrick' ya kwanza kwa Arsenal tangu Aaron Ramsey afunge katika mchezo wa Everton  Februari 2018.

Aubameyang aliyekosekana kwa mechi kadhaa ndani ya kikosi cha Arsenal kwa kile kilichoelezwa kuuguliwa na Mama mzazi, amerejea akiwa na nguvu nyingi na kutoa mchango mkubwa sana akichagizwa na mchango mkubwa wa winga kipepeo  Bukayo Saka.

Matokeo hayo yameifanya Arsenal inayofundishwa na Mikel Arteta kusogea  katika nafasi ya 10 miongoni mwa  timu 20 ikiwa na alama 34 katika michezo 24 iliyoshuka dimbani huku ikipoteza mechi mbili mfululizo kabla ya kushinda jana, urejeo wa Aubameyang umeongeza kitu kikubwa kwenye matokeo ya timu.

Aubameyang alijiunga na  Arsenal mwaka 2018 akitokea  Borussia Dortmund, tangu ajiunge ameichezea timu hiyo michezo 132 na kufunga magoli  81 na katika msimu huu ndani ya ligi kuu amecheza michezo 20 na kufunga magoli 8 yanayomfanya kufikisha  mabao 200 tangu kaanza kucheza soka la kulipwa Ulaya.