Jumamosi , 4th Nov , 2017

Mtibwa Sugar imepanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu soka Tanzania bara baada ya kutoa sare ya 0-0 dhidi ya Ndanda FC na kufikisha alama 17.

Mtibwa Sugar ilikuwa ugenini kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona kucheza mchezo wake wa raundi ya 9. Timu hiyo kutoka Turiani Manungu Morogoro haijapoteza mchezo hadi sasa ikijikusanyia alama 17 na kuwa miongoni mwa timu 4 za juu kwenye msimamo.

Ligi kuu leo imeendelea kwa michezo minne ya raundi ya 9 ambapo mabingwa watetezi Yanga wametoka sare ya 0-0 na Singida United. Njombe Mji na Mbao FC ya Mwanza zimetoka sare ya 0-0.

Mchezo mwingine wa leo ulikuwa ni Kagera Sugar ambayo imetoka sare ya 1-1 na Tanzania Prisons. Mtibwa sasa inashika nafasi ya pili nyuma ya Yanga ambazo zote zina alama 17 zikitofautiana idadi ya mabao.

Azam FC jioni hii inacheza na Ruvu Shooting kwenye uwanja wa Azam Complex na endapo itashinda itapaa kileleni huku timu zote zikisubiri matokeo ya kesho ya Simba na Mbeya City kwenye mchezo utakaopigwa jijini Mbeya.