Jumatano , 8th Jun , 2016

Mlinzi wa Kati wa kikosi cha Villarreal, Eric Bailly ndiye mchezaji wa kwanza kunyakuliwa na meneja mpya wa Manchester United Jose Mourinho .

Eric Bailly

Klabu ya Manchester United leo imeripotiwa kukamilisha upimaji wa afya wa beki wa kimataifa wa Ivory Coast Eric Bailly na kukamilisha usajili wake kutoka Villareal.

Wengi wa wapenzi wa soka hawakuwa wanamfahamu Eric Bailly kabla ya kuanza kuhusishwa na Man United mapema wiki hii.
Eric Bertrand Bailly alizaliwa eneo la Bingerville, Ivory Coast – sehemu sawa na aliyozaliwa mshambuliaji wa Manchester City Wilfried Bony.

Kipaji chake kilionekana na mtalaam kutoka klabu ya Espanyol Emilio Montagut wakati wa michuano ya vijana yaliyoandaliwa na kampuni ya Kihispania ya Promoesport huko Burkina Faso.

Ingawa aliwasili Cornella-El Prat mnamo December 2011, na kisha kuingia katika mfumo wa timu ya vijana wa chini ya miaka 17 wa Espanyol, ilikuwa miezi 10 kabla ya Bailly hajapewa kibali cha kufanya kazi.

Baada ya hapo akasubiri miezi 10 mingine kupata nafasi katika kikosi cha kwanza mnamo October 2014. Mechi ya kwanza ya soka la ushindani ilikuwa akiwa na miaka 20, ilikuwa mechi ya La Liga vs Real Sociedad, Espanyol wakashinda 2-0.

Ndani ya kipindi cha miezi minne tangu alipocheza mchezo wa kwanza wa La Liga, tayari alishapata nafasi ya kusajiliwa na Villareal na pia kuisadia timu yake ya taifa katika michuano ya African Cup of Nations.

Uhamisho huo ulifanyika wakati Bailly akiwa kwenye michuano ya AFCON ambayo mwishowe walishinda ubingwa akiwa ndio mchezaji mdogo zaidi kwenye kikosi cha Herve Renard, akiwa ametoka kupata nafasi kwenye kikoso cha timu ya taifa mwezi mmoja nyuma, Bailly alikuwa mmoja wa wafungaji penati waliofunga upande wa Ivory Coast katika mikwaju iliyoamua bingwa.