MO Dewji amlilia Hans Pope

Jumamosi , 11th Sep , 2021

Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya kampuni ya klabu ya Simba Sports Club, Mohammed Dewji ' MO' ameandika ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram kuelezea kwa upana mahusiano yake na marehemu Zacharia Hans Pope katika utimishi wake kwenye klabu ya Simba na kujivunia moyo wema alionao.

(Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa kampuni ya klabu ya Simba Sports Club, Mohammed Dewji (kushoto) alipokuwa na marehemu, Mjumbe wa bodi na Mwenyekiti wa kamati ya Usajili wa klabu hiyo Zacharia Hans Pope enzi za uhai wake.)

'MO' ameadika:

"Moyo wangu una maumivu makali sana. Bado ni vigumu kuamini na kukubali kuwa mjumbe wetu, kaka yetu, Zakaria Hans Poppe hatunaye tena."

"Kaka yangu, nimefanya kazi na wewe kwa miaka mingi, na kila siku uliweka maslahi ya Simba mbele. Kaka yangu ulikua na wema wa kipekee, na ulikua wa kwanza na ulinyooka linapokuja suala la kuilinda Simba, hukuwa na maslahi binafsi. Ulikua rafiki wa marafiki wa Simba, na ulikua tofauti na wasioitakia mema Simba."

"Kaka yangu, Umetangulia nasi tutafuata. Nitakukumbuka sana kaka yangu. Natoa pole sana kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki, pamoja na wanafamilia wote na mashabiki wa Simba kwa kumpoteza ndugu yetu.
Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi."

Mjumbe wa bodi ya wakurugenzi ya Simba SC Na Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu ya Simba, Zakaria Hanspope alifariki Dunia jana Septemba 10, 2021 katika hospitali ya Agha Khan alipokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.