Jumatano , 6th Mar , 2019

Kiungo wa klabu ya Ajax, Frenkie de Jong amefichua siri kwamba Barcelona ilimpa kazi ya kuhakikisha anaing'oa Real Madrid katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya wakati anafanya makubalano ya mkataba.

Ajax na Real Madrid

Amesema hayo kufuatia kufanikiwa kuiondoa Real Madrid katika hatua ya 16 bora ya Klabu Bingwa Ulaya usiku wa jana kwa jumla ya mabao 5-3, ambapo katika mchezo wa kwanza mjini Amsterdam, Real Madrid ilishinda kwa mabao 2-1 kabla ya hapo jana kuchapwa nyumbani Santiago Bernabeu kwa mabao 4-1.

De Jong alifanya makubaliano ya awali na klabu ya Barcelona msimu huu ambapo sasa atajiunga na miamba hiyo ya Catalonia msimu ujao.

Alipoulizwa kama alipewa ushauri wowote kuelekea mchezo huo wa marudiano, De Jong alijibu, "Oh wakati wa makubaliano ya mkataba wangu na Barcelona, waliniambia nijaribu kuiondoa Real Madrid katika michuano hii, kwahiyo hii itakuwa ni nzuri kwa Barcelona bila shaka".

Baada ya matokeo hayo, sasa Ajax inaungana na Tottenham Hotspurs kuwa timu za kwanza kuingia katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo huku Real Madrid iliweka rekodi ya kutofuzu hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2009/2010.

Michezo mingine miwili inatarajiwa kupigwa hii leo, ambapo PSG watakuwa nyumbani Parc de Prince kuikaribisha Manchester United, ambapo mchezo wa kwanza PSG ilishinda kwa mabao 2-0. Mchezo mwingine ni FC Porto itakuwa nyumbani kuikaribisha AS Roma huku ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza ugenini kwa mabao 2-1 katika mchezo wa mkondo wa kwanza mjini Roma.

Bofya hapa chini kuisikiliza zaidi.