Ijumaa , 17th Feb , 2017

Mchezaji wa zamani wa klabu ya Yanga, Prisons na Taifa Stars, Geofrey Bonny 'Ndanje' (37), amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jijini Mbeya alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kusumbuliwa kwa muda mrefu na maradhi ya kifua kikuu

Godfrey Bonny 'Ndanje'

Awali taarifa za kuugua kwa kiungo huyo zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, watu wakichangishana pesa kwa ajili ya kumsaidia mchezaji huyo kuendelea kupata matibabu katika hospitali hospitali ya Makandana - Tukuyu wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Dada wa mchezaji huyo aliyepewa nafasi katika timu ya Taifa Stas na kocha Marcio Maximo, Neema amesema, wamempoteza kipenzi chao baada ya kuhangaika naye kumuuguza kwa muda mrefu.

"Tumempoteza ndugu yetu ambaye amefariki usiku wa kuamkia leo, sisi tumekwenda majira ya saa 11:00 alfajiri tukakuta tayari amekwishafariki. Tumekuwa tukimuuguza kwa muda mrefu lakini Mungu amepanga yake, msiba upo nyumbani mjini Mbeya ambako taratibu za mazishi zimekwishaanza," amesema Neema Dada yake Marehemu Bonny.

Bonny alikuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars enzi za kocha Mbrazil, Marcio Maximo na wengi wanamkumbuka kwa soka lake maridadi katika sehemu ya kiungo, licha ya kwamba aliibuliwa wakati umri wake umekwishaenda.

Taifa Stars enzi za Marcio Maximo

Alicheza Yanga chini ya kocha Mserbia, Profesa Dusan Kondic na akaendelea hata alipoondolewa mwalimu huyo na kuletwa Mseribia mwingine, Kostadin Papic.

Ni kati ya wachezaji walioiwezesha Taifa Stars kukata tiketi ya kucheza fainali pekee za michauno ya Ubingwa wa Afrika (CHAN) zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.  

Hata hivyo, Maximo akamtema katika kikosi cha Stars baada ya fainali za CHAN nchini Ivory Coast mwaka 2009 kutokana na kuwa majeruhi.

Maumivu hayo yalimfanya aachwe na Yanga mwaka 2011 akaenda kumalizia soka yake Simrik SYC ya Nepal.     

 

Bonny akiwa hospitali akipatiwa matibabu hivi karibuni