Jumatano , 8th Aug , 2018

Mabingwa watetezi wa michuano ya Sprite Bball Kings Mchenga Bball Stars wamefanikiwa kutinga fainali ya pili mfululizo baada ya kuwafunga Portland kwenye game 3 ya nusu fainali iliyopigwa kwenye viwanja vya Don Bosco Oysterbay jijini Dar es salaam.

Mchenga Bball Stars (kijani) kweye mchezo wao dhidi ya Portland (nyeupe).

Mchenga Bball Stars wameibuka na ushindi wa pointi 81 dhidi ya 63 za Portland hivyo kuungana na Flying Dribblers katika fainali itakayokuwa na mechi 5. Mchenga na Portland zililazimika kufika game 3 baada ya game 1 na 2 kumalizika kwa kila timu kushinda game 1.

Katika mchezo wa leo mchezaji wa Mchenga Bball Stars Baraka Sadick amekuwa shujaa kwa timu yake baada ya kufunga pointi 36 kati ya 81 ilizopata leo. Pia amechukua rebound 1 na Assist 1. Kwa upande wa Portland Andrew Elias ndio amekuwa kinara kwa kufunga pointi 22, rebound 1 na Assist 1.

Baraka Sadick sasa amefikisha pointi 100 katika mechi 5 alizocheza kuanzia hatua ya 16 bora, robo fainali na mechi 3 za nusu fainali. Mechi za fainali ya michuano hiyo inayoandaliwa na East Africa Television LTD na kudhaminiwa na kinywaji cha Sprite zitaanza Jumamosi ya Agosti 18 kwenye uwanja wa taifa wa ndani.

Kwa upande wa Flying Dribblers wao walishinda mechi zao mbili kati ya tatu za nusu fainali dhidi ya Team Kiza hivyo kujikatia tiketi ya kucheza fainali baada ya msimu uliopita kuishia nusu fainali wakiwa na kumbukumbu ya kutolewa na Mchenga Bball Stars ambao wanakwenda kucheza nao fainali.