Jumatatu , 7th Sep , 2015

Uongozi wa Timu ya Mbeya City umesema unahitaji kuanza kupata point tatu kuanzia mchezo wa kwanza mpaka msimu unapomalizika katikia michuano ya ligi kuu itakayoanza kutimua vumbi Septemba 12 mwaka huu.

Katibu Mkuu wa Mbeya City Emmanuel Kimbe amesema wanaanzia nyumbani lakini wao wamejipanga kwa ajili ya msimu mzima na wamepania kuanza kuondoka na point tatu katika mchezo wa kwanza kwani kikosi chao msimu huu kimefanya usajili wa uhakika, ingawa kutakuwa na mabadiliko.

Kimbe amesema ushindani utakuwa mkubwa kwa mwaka huu lakini watajitahidi kuwa tofauti na msimu uliopita ambapo kwa misimu miwili katika mechi za ufunguzi hawakuondoka na point.

Utakuwa msimu wa tatu kwa timu hiyo ambayo safari hii itaanzia tena nyumbani kama misimu miwili iliyopita licha ya kushindwa kuondoka na ushindi na kuambulia sare mara mbili ambapo msimu wa kwanza wa mwaka 2013/14 walifungua dhidi ya Kagera Sugar na walitoka sare ya 0-0, msimu uliofuata dhidi ya JKT Ruvu 0-0 kwenye uwanja huohuo na safari hii wanafungua kwa mara nyingine na Kagera Sugar.