Mwalimu Mayanga anachukua nafasi ya Mecky Maxime aliyekuwa kocha mkuu wa Mtibwa na ambaye msimu huu ameingia mkataba wa kuifundisha klabu ya Kagera Sugar.
Mayanga atasaidiwa na Patrick Mwangata pamoja na Zuberi Katwila ambao tangu awali walikuwemo kwenye benchi la ufundi la Mtibwa kama walimu wasaidizi.
Mwalimu Mayanga ambaye msimu uliopita aliifundisha klabu ya Prisons ya Mbeya na kuiwezesha kumaliza katika nafasi ya nne, ni mmoja wa makocha wenye ujuzi mkubwa na uzoefu hapa nchini.
Hii ni mara ya pili kwa Mwalimu Mayanga kuifundisha klabu ya Mtibwa Sugar kama mwalimu mkuu. Mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 2008/09 na 2009/10 ambapo aliweza kuipatia klabu ya Mtibwa mafanikio makubwa kwa kuiwezesha kutwaa kombe la Tusker, Kombe la Mapinduzi na pia kutwaa ngao ya jamii.
Kocha Mayanga ana leseni ya ukocha ya daraja A inayotambuliwa na CAF, na pia aliwahi kuhudhuria kozi ya kimataifa ya ukocha wa mpira wa miguu iliyofanyika kwa wiki tatu nchini Ujerumani mwaka 2009.





