Jumapili , 1st Jun , 2014

Mkutano mkuu wa wanachama wa klabu ya yanga umekutana leo jijini DSM na kufanya marekebisho katika baadi ya vipengele vya katiba ya klabu hiyo.

Mamia ya wanachama wa Yanga waliojitokeza katika mkutano mkuu uliofanyika leo katika ukumbi wa bwalo la polisi Oysterbay.

Mkutano Mkuu wa marekebisho ya baadhi ya vipengele kwenye Katiba ya Yanga umefanyika na kumalizika salama na furaha kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi -Oysterbay huku wanachama wakipitisha kipengele cha kuundwa kwa kamati ya maadili.

Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo inasema kuwa wanachama hai wapatao 1,560 wamepitisha kipengele hicho kipya kwa ajili ya maslahi na faida ya Wana Yanga kwani bila kufanya hivyo timu isingeweza kuruhusiwa kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Aidha katika mkutano huo Uongozi wa Yanga umewatoa hofu wanachama kwa kuwaambia kuwa usajili unaendelea kufanyika na nafasi zilizobakia ni nne tu hivyo pindi utakapokamilika basi uongozi utaweka wazi kila kitu.

Kuhusu nafasi ya Kocha Mkuu Uongozi umesema kuwa Kamati ya Mashindano imekwisha kabidhi mapendekezo yao na kwa sasa upo kwenye mazungumzo na Marcio Maximo aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa Tanzania kuja kukinoa kikosi cha Jangwani.

Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini Mama Fatma Karume aliongoza kikao cha waachama kilichomuomba Mwenyekiti wa sasa kuendelea na uongozi ambapo mwenyekiti huyo alitoka nje na kamati yake ya utendaji na pindi waliporejea walikubali ombi hilo na kusema watafuata taratibu za kikatiba.

Mwisho kupitia mkutano mkuu wa leo wa wanachama umeazimia kuwaongezea muda wa mwaka mmoja Mwenyekiti pamoja na Makamu wake Clement Sanga ili waweze kukamilisha masuala ya katiba na kuweza kuandaa mkutano wa uchaguzi baada ya katiba kupitishwa na TFF.