Alhamisi , 16th Feb , 2017

Mshambuliaji wa Simba, raia wa Burundi, Laudit Mavugo, ameendelea kuwa moto baada ya leo kuifungia Simba bao moja na la pekee dhidi ya African Lyon na kuivusha hadi hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho la TFF.

Laudit Mavugo

Katika mchezo huo wa kwanza wa raundi ya 16 bora uliopigwa katika dimba la Taifa Dar es Salaa, African Lyon wameonesha ushindani mkubwa licha ya kuzidiwa uwezo kwa kiasi kidogo na Mnyama, na hatimaye kumaliza dakika 45 za kwanza kukiwa hakuna bao.

Katika kipindi cha pili Simba walizidisha mashambulizi kupitia kwa nyota wake Shiza Kichuya, Mavugo, na Ajibu, na hatimaye Mavugo akaitendea haki pasi ya Ajibu na kuipatia Simba bao katika dakika ya 57.

Hadi mwisho wa mchezo Simba imemaliza kwa kumiliki mpira kwa asilimia 59 huku African Lyon ikimiliki kwa asilimia 41 ikiwa haijapiga mashuti yoyote yenye madhara langoni kwa Simba.

Simba Vs African Lyon, Taifa

Kwa mara ya kwanza leo baada ya kukosekana kwenye michezo kadhaa, Nahodha Jonas Mkude, na Mohamed Ibrahim wamecheza katika mchezo wa leo, ambapo Mo, alichukua nafasi ya Said Ndemla

Mara baada ya mchezo huo, nahodha wa African Lyon Jafary amesema hawajafurahia matokeo hayo na kuwataka mashabiki wao wasikate tamaa huku Nahodha wa Simba Jonas Mkude akisema kilichowabeba leo ni maandalizi mazuri, na kuwataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuisapoti timu yao hata pale inapofanya vibaya.

Simba sasa inasubiri mpinzani wake atakayepangiwa baadaye, baada ya kumalizika kwa raundi ya 16 bora.