Jumanne , 1st Dec , 2015

Mashirika na Taasisi binafsi pamoja na serikali zimeaswa kurejesha na kuhamasisha michezo katika maeneo mbalimbali ili kuibua vipaji na kuwapa ajira vijana kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

Meneja wa timu ya misitu Saohil ya mkoani Iringa Said Aboubakari amesema wao kama taasisi ya serikali wameamua kujikita kwenye michezo ili kutoa elimu ya umuhimu wa utunzaji wa misitu na pia kuwapa ajira vijana ambao wana uwezo wa kucheza na kuipandisha timu yao madaraja ya juu.

Aboubakari amesisitiza kuwa endapo mashirika hayo yatawekeza kwenye michezo Tanzania itaondokana na jina la kichwa cha mwendawazimu ambalo limeendelea kutumiwa hivi sasa kutokana na hali halisi ya klabu na timu yetu ya taifa kufanya vibaya kwenye mashindano ya kimataifa.

Timu ya Saohil imecheza mechi za kirafiki na timu za vijana za Yanga na Azam katika ziara yao inayoendelea jijini Dar es salaam kwa wiki moja.