Alhamisi , 28th Jan , 2016

Walinda mlango wawili wa kituo cha kukuza vipaji cha magolikipa nchini TGTC wanatarajiwa kuelekea nchini Msumbiji kwa ajili ya majaribio ya wiki moja katika timu za ligi kuu nchini humo.

Mkurugenzi wa kituo hicho Peter Manyika amesema, kituo chake kinatoa walinda mlango wawili ambapo mmoja ambaye ni Said Kipao anatarajiwa kuondoka mapema kesho ambapo atafanya majaribio na timu ya Qual Money iliyo mji wa Premeiro nchini humo huku Daudi Mwasongwa akitarajiwa kuondoka siku ya Jumatatu ambaye anafanya majaribio na timu ya Polisi ya nchini humo iliuo mji wa Nampula.

Manyika amesema, vijana hao iwapo watafuzu katika majaribio watasaini mikataba moja kwa moja tayari kwa ajili ya kuanza kazi na timu huzo.

Manyika amesema, vijana hao waliandaliwa kwa muda mrefu ikiwa ni sehemu ya kucheza kimataifa zaidi na mpaka sasa bado wanaendelea kuwaandaa vijana wengine ili kuweza kupata magolikipa wengi zaidi ambao wataweza kuitangaza nchi katika ramani ya soka.

Kwa upande wake Kipao ambaye anatarajiwa kuondoka nchini kesho amesema juhudi, nidhamu, kujituma pamoja na uvumilivu ndio vimemfanya kufikia katika hatua hiyo ya kuweza kufanya majaribio katika timu ya nje ya nchi.

Kipao amesema, lengo lake ni kuweza kuipeperusha bendera ya nchi na kuwavutia mawakala ili waweze kurudi tena nchini kwa ajili ya kuweza kutafuta vipaji vingine vitakavyoweza kuongeza idadi ya watanzania wanaocheza soka la nje ya nchi.