
Kocha David Moyes aliyetimuliwa Man U baada ya kuinoa kwa miezi 10 tu
Klabu ya Machester United leo imemfukuza kazi meneja wake David Moyes baada ya kuinoa timu hiyo kwa miezi kumi na mchezaji Ryan Giggs ameteuliwa kuinoa timu hiyo mpaka mwisho wa msimu.
Moyes akiwa na timu hiyo ya Machester aliiongoza katika michezo 51 na kushinda michezo 27 na kutoka sare michezo 9 na kufungwa michezo 15 ushindi ukiwa asilimia 52.9.
Moyes, ambaye anatimiza umri wa miaka 51 Ijumaa hii, aliteuliwa kwa mapendekezo ya Mscoti mwenzake Ferguson, aliyestaafu mwishoni mwa msimu uliyopita baada ya kuitumikia klabu ya Manchester United kwa miaka 26.
Ferguson aliiongoza klabu hiyo katika ushindi taji lake la 13 chini ya uongozi wake, na la 20 kwa jumla. Kuondoka kwa ghafla kwa Moyes kumerejesha kumbukumbu za kipindi kibaya ilichokipitia klabu hiyo ya Old Trafford kati ya mwaka 1969 na 1971, kufuatia kustaafu kwa Matt Busby, baada ya kuiongoza kwa miaka 24.