Jumatano , 26th Dec , 2018

Kampeni ya michuano ya Mapinduzi Cup inatarajia kuanza kutimua vumbi Januari Mosi na kumalizika Januari 13 katika visiwa vya Zanzibar.

Azam FC wakishangilia ubingwa wa Mapinduzi 2018

Michuano hiyo ambayo bingwa wake mtetezi hivi sasa ni Azam FC, itahusisha jumla ya timu 9 ambapo timu tatu ni kutoka Tanzania Bara na sita za visiwani humo.

Mchezo wa kwanza kabisa utakaopigwa Januari mosi ni kati ya KVZ na Malindi huku bingwa mtetezi Azam FC akishuka dimbani dhidi ya Jamhuri,  Januari 2.

Yanga watashuka dimbani Januari 03 kumenyana na KVZ wakati Simba wao wakivaana na Chipukizi, Januari 4.

Kwa mujibu wa kamati ya maandalizi ya mashindano hayo, zawadi kwa mshindi wa kwanza itaongezwa kutoka milioni 10 mpaka milioni 15 ikiwa ni pamoja na medali za dhahabu pamoja na kombe.

Mashindano hayo yatatumia viwanja viwili, uwanja wa Amaan ambao utachezwa mechi za mawanzo hadi hatua ya nusu fainali na uwanja wa Gombani ambao utachezwa mechi ya fainali pekee.