Robert Lewandoski alifunga hat-trik na kuipaisha Barcelona kileleni katika msimamo wa La Liga kwa tofauti ya pointi tatu mbele ya Mahasimu wao wakubwa Real Madrid kutokana na ushindi walioupata ugegeni dhidi ya Deportivo Alaves.
Ushindi wa Real Madrid siku ya Jumamosi katika dimba la Santiago Barnabeu dhidi ya Villareal uliwafanya kufikisha alama sawa na kikosi cha Hansi Flick kabla ya kucheza jana dhidi ya wapinzani wao wanaotoka jiji moja la Barcelona.
Miamba ya Catalunya ambayo ilipoteza mchezo wao uliopita dhidi ya Osasuna, walionekana wanahitaji ushindi kwa kiasi kikubwa walifunga mapema kupitia kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Polandi Lewandoski baada ya kupokea pasi kutoka Rafinha.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 36, alifunga goli lake la pili kwa kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Mbrazil aliye katika kiwago bora sana kiuchezaji tangu ujio wa kocha raia wa Ujerumani ndani ya Barca.
Goli la tatu walilofunga Barcelona, limetokana pasi ya Eric Garcia kwa mshambuliaji wao hatari aliyewahi kuzitumikia Borrusia Dortmund na Bayern Munich zote za nchini Ujerumani raia wa Polandi.
Lewandoski mpaka sasa ameshafunga goli 13 katika michezo 11 ya mashindano yote akiwa na jezi ya mabingwa wa La Liga msimu wa 2022-2023 wenye wastani wa kufunga goli tatu au zaidi kwenye michezo ya ligi kuu nchini Hispania msimu huu.