Jumatano , 25th Jan , 2023

Ladies First ikiwa ni wazo la Nguli wa Riadha nchini Tanzania, Kanali mstaafu Juma Ikangaa, imefanyika mwaka huu ukiwa ni msimu wa nne na kushirikisha mikoa 30 Kati ya 31 Tanzania Bara na Visiwani.

Ladies First ikiwa ni wazo la Nguli wa Riadha nchini Tanzania, Kanali mstaafu Juma Ikangaa, imefanyika mwaka huu ukiwa ni msimu wa nne na kushirikisha mikoa 30 Kati ya 31 Tanzania Bara na Visiwani.

Mwaka huu, mashindano hayo yalifanyika January 21 na 22 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na kushirikisha zaidi ya wanariadha 186.

Kanali Mstaafu Ikangaa, ambaye enzi zake aliiwakilisha vema Tanzania kimataifa katika mbio za marathoni, ikiwemo nchini Japan, nchi hiyo imekuwa ikimuenzi na kumpa heshima kubwa ambapo hivi sasa ni Balozi wa Hiari wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).

Katika kumuenzi Kanali Ikangaa, Japan ilimtaka kusema kitu ambacho nchi hiyo iifanyie Tanzania, ndipo kwa kushirikiana na wadau wake mbalimbali, akaja na wazo la kuwaenzi na kuhamasisha wanawake kushiriki katika mchezo wa Riadha, hasa ikizingatiwa medali ya kwanza ya kimataifa Tanzania ililetwa na Mwanamke Theresia Dismas mwaka 1964, katika michezo ya All Africa nchini Congo Brazzaville, kupitia mchezo wa Kurusha Mkuki 'Javelin'.

Wazo hilo lilianza kutekelezeka mwaka 2017 kwa mashindano yaliyofanyika Uwanja wa Taifa, sasa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ambapo baadhi ya washindi wamekuwa wakipata nafasi ya kwenda kushiriki mbio za Nagai City nchini Japan.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa Tanzania (BMT), Bi. Neema Msitha, aliipongeza JICA na kampuni mbalimbali za Kijapan zinazofanya kazi nchini, Kanali Ikangaa,serikali ya Tanzania na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), kwa kufanikisha mashindano hayo kwa msimu wa nne sasa.

Bi. Msitha, anasema mashindano hayo yalianza mwaka 2017 na kufanyika kwa mafanikio makubwa miaka mitatu mfululizo hadi 2019 kabla kusitishwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo janga la UVIKO 19 'Covid 19'.

"Lengo la mashindano haya ni kuhamasisha ushiriki wa watoto wa kike katika michezo hususan Riadha, kutoa fursa kwa wanariadha wa kike kuonyesha vipaji vyao na kuendeleza vipaji vya wanariadha ambao wataiwakilisha nchi katika mashindano ya kitaifa na kimataifa," anasema Bi. Msitha.

Tangu kuanza kwa mashindano hayo mwaka 2017, Wanariadha wa Tanzania na viongozi wao, wamekuwa wakipata nafasi ya kwenda kushiriki Nagai Marathon, ambapo wanariadha akiwemo Angel John Joseph Yumba, Fabian Nelson Sulle, Fabian Joseph, Alphonce Felix Simbu na wengineo wameweza kung'ara.

Mbali na hilo, Ladies First iliweza kuishirikisha nchi ya Sudan Kusini na kushiriki mashindano ya mwaka 2019 jijini Dar es Salaam.

Mwaka huu 2023, Ladies First imezidi kufungua milango katika mchezo wa Riadha Tanzania, ambapo Sudan Kusini iliwakilishwa na viongozi wake mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Michezo nchini humo, Peter Baptist, Balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania, Deng Abel na wengineo.Baptist katika salamu zake, mbali na kushukuru na kupongeza Tanzania kwa mashindano hayo, anasema na kwao wana mashindano kama hayo yajulikanayo kama 'Umoja na Amani', yakilenga kutumia michezo kuhamasisha amani na umoja katika Taifa hilo ambalo liliandamwa na vita miongoni mwao kwa miaka kadhaa.

Mwakilishi huyo, anasema katika kuendeleza ushirikiano na Tanzania, wanatoa mwaliko kwa wanariadha wanne waliofanya vizuri katika Ladies First 2023 wa mbio tofauti ukiondoa mita 5000 kwenda Sudan Kusini kushiriki mashindano hayo yanayotarajiwa kufanyika miezi miwili ijayo.

Mbali na fursa hizo zilizojitokeza Ladies First 2023, nyingine ni kwa Mwanariadha anayefanya vema hivi sasa, Mshindi wa Medali ya Fedha Common Wealth Games 2022, Alphonce Simbu, naye kuteuliwa kuwa Balozi wa Hiari JICA, akiungana na Kanali mstaafu Ikangaa.

Haya ni kati ya mafanikio ya Ladies First 2023, na hakika uwajibikaji ukizidi kuongezeka, bila shaka milango zaidi itazidi kufunguka katika medani ya riadha Tanzania.