Jumatatu , 4th Jul , 2016

Mafunzo ya ukocha wa mpira wa meza daraja la pili yanayotambuliwa Shirikisho la Mpira wa Meza Duniani ITTF yameanza rasmi hii leo kwa kushirikisha mikoa ya Tanzania na Zanzibar pekee.

Katibu wa Chama cha Mpira wa Meza nchini TTTA Issa Mtalaso amesema, hapo awali walitarajia kupata washiriki kutoka nchi za Falme za Kiarabu, Nigeria na Kenya lakini wameshindwa kushiriki kutokana na sababu ya mfungo wa mwezi wa Ramadhan.

Mtalaso amesema, kozi hiyo itakuwa ya siku nane ambapo inaendeshwa na mkufunzi Ahmed Dawlatly kutoka nchini Misri.

Mtalaso amesema, mara baada ya kumaliza mafunzo hayo, washiriki watakuwa na saa 48 ya kufundisha chini ya usimamizi wa kiongozi wa TTTA atakayechaguliwa na mara baada ya kumaliza watajaziwa fomu ambazo zitatumwa ITTF ambayo ndiyo itakayoandaa vyeti kutokana na ufaulu watakaoupata.

Mafunzo hayo ambayo ni ya mara ya kwanza kwa hapa nchini yanatarajiwa kufanyika tena hapo mwakani kwa upande wa walimu ikiwa ni sehemu ya kukuza mchezo huu kuanzia kwa vijana hapa nchini.