Ijumaa , 11th Feb , 2022

Hatua ya 16 bora ya michuano ya Azam Sports Federation Cup inatarajiwa kuanza kesho Februari 12 kwa michezo miwili, moja ya mchezo ni Baga Friends dhidi ya Azam FC. Kocha wa Azam FC Abdi Hamid ametoa tahadhari kuwa mechi dhidi ya timu ndogo huwa zinakuwa ngumu.

Kocha wa Azam FC Abdi Hamid Moallin kulia

Kuelekea mchezo wao dhidi ya Baga Friends, Kocha mkuu wa Azam fc Abdi Hamid Moallin amejinasibu kuendelea kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ambayo inatoa mwakilishi kwenye michuano ya kimataifa kwa upande wa Tanzania bara.

"nadhani wachezaji wako tayari na wanajua mchezo wa FA huwa inakuwaje, ni matumaini yetu tutashinda mchezo wa kesho na kufuzu kwenda hatua inayofuata maana kucheza na timu ndogo kwenye kombe la FA mara nyingi huweza kusababisha mshangao ,na kwa Baga friends hakuna tofauti ''. amesema Moalin

Azam ambao walitwaa kombe hilo msimu wa 2018/19 kwenye uwanja wa Ilulu mkoani Lindi baada ya kuifunga klabu ya Lipuli FC ya mkoani Iringa kwa bao 1-0 goli la mzambia Obrey Chirwa huku msimu uliopita wakiondoshwa katika hatua ya nusu fainali na klabu ya soka ya Simba kwa kichapo cha goli 1-0, mchezo uliofanyika katika uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.

Mchezo mwingine wa hatua hii ya mtoano unaochezwa kesho Mbuni Fc ya Arusha itaminyana na klabu ya Geita Gold majira ya 10:00 Jioni.