Alhamisi , 28th Mei , 2015

Kesi inayomkabili kipa mkongwe Juma Kaseja Juma dhidi ya Yanga, imeshindwa kumalizika hapo jana baada ya Mahakama ya Kazi Kitengo cha Uamuzi kuipiga kalenda kwa mara nyingine hadi juni 16 mwaka huu.

Uongozi wa Yanga umemfungulia mashtaka kipa huyo wa zamani wa Simba kwa madai ya kukiuka masharti ya mkataba kati yake na klabu hiyo ya Jangwani alipoamua kuikacha baada ya kupishana kauli na uongozi.
Kaseja alidai kutolipwa kwa wakati mwafaka sehemu ya fedha za ada za usajili wake kwa mabingwa hao mara 25 wa Tanzania Bara ambapo katika kesi hiyo, Mahakama ya Kazi imeshindwa kutoa uamuzi kutokana na wakili wa Kaseja, Samson Mbamba kutofika mahakamani.

Kwa upande wa kesi inayomkabili mshambuliaji Geilson Santos Santana ‘Jaja’ dhidi ya Yanga, mahakama pia imeipiga kalenda kesi hiyo kutokana na upande wa mlalamikiwa (Jaja) kutowafika mahakamani ambapo kama Jaja hatatokea mahakamani mara tatu, kesi italazimika kusikilizwa upande mmoja na kutolewa uamuzi.