Alhamisi , 26th Jul , 2018

Msajili wa Vyama vya Michezo nchini, Ibrahim Mkwawa, amesema katiba ya Simba iliyosajiliwa mwaka huu 2018 baada ya mapendekezo kutoka kwa wanachama ndiyo itakayotumika katika uchaguzi mkuu ujao.

Msajili wa Vyama vya Michezo nchini, Ibrahim Mkwawa.

Mkwawa amesema katiba mpya ya Simba iliyosajiliwa siku chache zilizopita imefuata taratibu zote mpaka serikali ikaamua kuipitisha ndiyo itakayotumika kwenye uchaguzi na si vinginevyo.

"Simba wameshakamilisha usajili wa katiba mpya ambayo imefuata taratibu zote, hivyo itakayotumika kwenye uchaguzi ujao ni hii ya 2018 na si vinginevyo" amesema.

Katiba hiyo ilifanyiwa mabadiliko kutoka ile ya zamani ya mwaka 2014 iliyokuwa inamtaka mgombea Urais kuwa na kiwango cha elimu ya kidato cha nne lakini hii ya sasa inamtaka awe na shahada ama digrii.

Simba walifanya mabadiliko hayo ambayo yaliyokuwa ni mahususi kwa ajili ya kuupokea mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu hiyo ambayo tajiri kijana, bilionea Mohammed Dewji Mo, amewekeza hisa zenye thamani ya bilioni 20.

Simba inatarajia kukutana Julai 31 kwa ajili ya kuanza mchakato mzima wa kumpata Rais mpya wa klabu hiyo ambaye ambaye atakuwa madarakani kwa miaka minne ijayo. Kwa sasa Simba inaongozwa na Kaimu Rais, Salim Abdallah 'Try Again' kutokana na Rais wake, Evans Aveva kuwa mahakamani kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha.