Katibu wa TSA, Ramadhani Namkoveka amesema,wameamua kuwa na kambi ya nje ya nchi kwa waogeleaji ambao watashiriki mashindano ya Olimpiki ili kuendana na hali ya mazingira ya kimichezo kwani Tanzania haina miundombinu ya kutosha ya mchezo wa kuogelea kwa ajili ya maandalizi ya vijana hao.
Namkoveka amesema, waogeleaji wanapata maeneo ya kufanyia mazoezi katika shule hapa nchini lakini muda unakuwa hautoshi kwa sababu wanatakiwa muda mrefu takribani masaa mawili kufanya mazoezi ikiwa ni mara mbili kwa siku na pia kwa upande wa bwawa linatakiwa la Mita 50 na Tanzania hamna bwawa lenye urefu huo.
Namkoveka amesema,waogeleaji hao ambao ni Hilary Hilary ambaye yupo nchini Dubai na Magdalena Moshi ambaye yupo nchini Australia wanatarajia kuwasili nchini kati ya Julai 25 na 28 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya safari ya kuelekea Rio nchini Brazili katika mashindano ya Olimpiki yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agasti 05 mwaka huu.



