Jumatano , 21st Oct , 2015

Michuano ya Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara inaendelea hapo kesho kwa mechi nne kuchezwa ambapo Jkt Ruvu itaikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Karume jijini Dar es salaam huku Azam Fc ikiwa ugenini dhidi Ndanda Fc Uwanja wa Nangwanda sijaona.

Kocha wa Timu ya JKT Ruvu ambayo itawakaribisha watengeneza Sukari wa Mtibwa Sugar ya Mkoani morogoro Uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, Abdallah kibaden Mputa amesema anapata tabu katika kupanga kikosi cha kwanza katika mechi hiyo kutokana na kutowajua vizuri wachezaji wake.

Kibaden amesema, wanatarajia kushinda lakini anafanya kazi kwa kufuata maelekezo ya mtu anayewajua wachezaji kwani timu hiyo kaichukua ikiwa imecheza mechi sita bila kuwa na mafanikio yoyote hivyo mpango wake ni kuweza kuisadia Jkt na kuweza kufikia malengo.

Kwa upande wake nahodha msaidizi wa Timu hiyo Michael Aidan amesema, wanaimani watapata ushindi katika mechi ya kesho kutokana na maandalizi pamoja na kocha kurekebisha mapungufu yaliyokuwa yakionekana kupunguza kasi ya uchezaji katika timu.

Aidan amesema, mabadiliko ya kocha hayachangii timu kushuka au kupanda kwa kiwango cha uchezaji lakini kinachotakiwa ni kurekebisha mapungufu waliokuwa nayo katika mechi zilizotangulia na kocha ameshayafanyia kazi pamoja na wachezaji kuendana na kasi ya Ligi iliyopo msimu huu.

Mechi nyine ambazo zitapigwa hapo kesho ni Mwadui FC watawakaribisha Mgambo Shooting katika uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga huku huko Jijini Mbeya, Mbeya City watawakaribisha African Sports katika uwanja wa Sokoine ambapo baada ya hapo Ligi hiyo itasimama ili kuweza kupisha zoezi la Uchaguzi Mkuu wa nchi.