Ijumaa , 11th Feb , 2022

Rais na mtendaji mkuu wa mchezo wa mbio za magari ya Langa langa (Formula 1) Stefano Domenicali amethibitisha kuwa wamesaini mkataba na taifa la Bahrain mpaka mwaka 2036 ambapo taifa hilo litakuwa sehemu ya mataifa yatakayo andaa mbio hizo kwa miaka 14.

Kwa mara ya kwanza Bahrain waliandaa mbio za F1 mwaka 2004

Taifa la Bahrain kwa mara ya kwanza waliaandaa mbio za Langa langa (F1) mwaka 2004 na lilikuwa taifa la kwanza kutoka Mashariki ya kati kushiriki kwenye mchezo huu.

Baada ya kusaini mkataba huo mpya  Rais na Mtendaji mkuu wa Formula 1 Stefano Domenical amesema,

‘’Bahrain ilikuwa nchi ya kwanza ukanda wa Mashariki ya Kati kukaribisha Formula 1 na ina nafasi ya pekee sana katika mchezo wetu, na mimi binafsi nataka kumshukuru HRH Prince Salman na timu yake kwa kujitolea na bidii yao katika ushirikiano wetu na tunatazamia miaka mingi ya mbio mbele yetu." Amesema Stefano Domenical

Mpaka sasa jumla ya mbio 14 zimeshafanyika katika taifa hilo ambapo kampuni ya magari ya Mercedes ya Ujerumani ndio imeshinda mara nyingi zaidi mara 7 na Lewis Hamiliton dereva wa kampuni hiyo ameshinda mara 5 ikiwa ni mara nyingi kuliko madereva wote tangu mwaka 2004.

Na mbio za kwanza za msimu huu za Langa langa zitafanyika Bahrain na msimu mpya utaanza kutimua vumbi Machi 20 mwaka huu na msimu utamalizika Novemba 20, 2022.