Alhamisi , 22nd Sep , 2022

Klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani inaripotiwa kuwa imejipanga kumuuza kiungo wao raia wa England mwenye umri wa miaka 19 Jude Bellingham kwa ada ya uhamisho ya Euro milioni 150 zaidi ya Shilingi Bilioni 344 kwa pesa ya Tanzania.

Jude Bellingham ana umri wa miaka 19 anacheza nafasi ya kiungo

Bellingham ni moja kati ya wachezaji vijana wenye vipaji vikubwa na anawaniwa na vilabu kadhaa vikubwa barani Ulaya ambavyo vimeonyesha nia yakutaka kumsajili. Vilabu hivyo ni Chelsea, Manchester United, Liverpool ambao wanatajwa wameshaanza mazungumzo na mchezaji huyo, Manchester City na Real Madrid.

Lakini kwa mujibu wa ripoti kutoka nchini ujerumani zinadai kuwa matamanio ya mchezaji huyu ni kujiunga na Real Madrid na ataipa kipaumbele endapo kama mabingwa hao wa Ulaya wataonyesha nia ya moja kwa moja yakutaka kumsajili.

Mkataba wa kinda huyo wa England na klabu yake ya Borussia Dortmund unamalizika mwaka 2025, taarifa kutoka nchini Ujerumani zinadai kuwa Dortmund wapo tayari kumuuza mchezaji huyo baada ya kupita mwaka 2023 na watamuuza kwa dau la Euro milioni 150 kama ada ya uhamisho ambayo ni zaidi ya Bilioni 344 kwa pesa ya Tanzania.