Jumanne , 17th Jan , 2023

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha, amewasihi mabondia nchini kuwa na nidhamu ili kuaminiwa na jamii pamoja na kuwavutia wadhamini kuwekeza katika mchezo huo

Msitha amesema hayo wakati akizungumza na bondia Pius Mpenda na ujumbe alioambatana nao walipotembelea ofisi za BMT kushukuru kwa ufadhiliwa tiketi 3 za ndege kurejea nyumbani baada ya kuibuka na ubingwa wa mkanda wa WBU - Afrika (Middleweight) katika pambano la round 12 lililofanyika nchini Uganda dhidi ya Bondia Farouk Daku.

Amesema kuwa, kufanya kwao vizuri kutasaidia kulipa fadhila kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Hassan Suluhu ambaye ameamua kuipa mchango wa kuiendeleza tasnia ya michezo hapa nchini.

“Tunawapongeza mabondia wachache ambao wamekuwa wanaiwakilisha nchi vizuri, lakini tumekuwa hatupati taarifa zao mbaya, hatukatai kunaweza kuwepo na changamoto kwa upande wa kamisheni ama Serikali ni vyema tukatumia njia nzuri ya kuwasilisha matatizo yetu,” amesema Neema.

Aidha amewaagiza Kamisheni ya Ngumi za kulipwa Tanzania (TPBRC) kuhakikisha mabondia wanakuwa na mameneja, na kuwataka wawe wanawaandalia semina wadau wao hao pamoja na makocha.

Kwa upande wake Bondia Pius Mpenda ameishukuru Serikali kwa kumpa sapoti ambayo hakuitarajia na ameahidi kuutumia mkanda huo kupambana na mabondia wa ndani na nje kuendelea kuonyesha ubora wake.

Naye Katibu Mkuu wa TPBRC Yahya Poli, alisema kuwa wana mpango wa kuendesha kozi ya waamuzi na makocha wa mchezo huo.

Meneja wa bondia huyo, Hassan Seta ameiomba Serikali kuendelea kusapoti wadau wa ngumi wenye vituo vya kukuza vipaji vya mabondia ili waweze kuibua vipaji zaidi.