
Zlatan ameifikia rekodi ya kufunga mabao 500 kwa ngazi ya klabu na timu ya taifa kwenye mchezo wa ligi kuu ya soka nchini Marekani (MLS) ambao LA Galaxy ilishinda kwa mabao 5-3, wikiiendi iliyopita.
Beckham ambaye aliwahi kucheza pamoja na Zlatan katika klabu ya PSG ameisifia rekodi yake ya ufungaji huku akimtania kuwa sasa ameonesha ukongwe wa kweli katika soka.
Idadi hiyo ya magoli ya Zlatan Ibrahimovic imemfanya kuwa ni mchezaji wa tatu anayecheza soka hadi sasa kufikisha magoli 500 akiungana na nyota wakubwa duniani kama Lionel Messi na Cristiano Ronaldo.
" Zlatan, ninakupongeza kwa rekodi hiyo uliyoifikia ", amesema Beckham katika video iliyorushwa na klabu ya LA Galaxy.
" Magoli 500 ni safari kubwa, ni mchezaji mkubwa, ni mafanikio makubwa, najivunia kucheza na wewe na pia kucheza dhidi yako, najivunia kuwa rafiki yako mzuri ", ameongeza.
Zlatan Ibrahimovic ambaye ni raia wa Sweden alianza kucheza soka katika klabu ya Malmo ya nchini kwao, akifunga mabao 18, kisha kujiunga na Ajax na kufunga mabao 48 na kuhamia Juventus ambako alifunga mabao 26.
Baada ya kutoka Juventus alijiunga na Inter Milan ambayo aliifungia mabao 66 kisha kujiunga na Barcelona na kuifungia mabao 22 kabla ya kurejea tena nchini Italia katika klabu ya AC Milan ambako alifunga jumla ya mabao 56 na baadaye kuhamia PSG ambako aliacha rekodi ya kuwa mfungaji bora wa klabu hiyo kwa mabao yake 156, rekodi ambayo imevunjwa na Edinson Cavani mwezi Januari mwaka huu. Baada ya kuondoka PSG, Zlatan alijiunga na Man United ambayo aliifungia mabao 29 na kuhamia LA Galaxy aliko hadi hivi sasa.