Ijumaa , 23rd Oct , 2015

Chama cha mpira wa kikapu mkoa wa Dar es salaam BD kimesema kinatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu wa viongozi baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa nchi unaotarajiwa kufanyika Jumapili wiki hii.

Mwenyekiti wa BD Mwenze Kabinda amesema uchaguzi wa BD ulitakiwa kufanyika June mwaka huu lakini walishindwa kutokana na maandalizi ya mashindano ya kimataifa ya Mpira wa Kikapu.

Kabinda amesema, uchaguzi wao unasimamiwa na ofisi ya michezo mkoa kupitia kwa afisa michezo mkoa hivyo wakashauriwa kupeleka uchaguzi wa chama baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa nchi.

Kabinda amesema, baada ya uchaguzi mkuu wa nchi watatoa maelezo ya siku 60 kwa mujibu wa katiba ili kuweza kuwataarifu wadau juu ya uchaguzi huo wa viongozi mbalimbali wa chama hicho utakaofanyika ndani ya siku 60 zitakazotangazwa.