Jumamosi , 27th Jan , 2018

Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa ligi kupitia kwa Afisa Mtendaji mkuu wa Bodi ya ligi Boniface Wambura imetangaza kuipiga faini ya shilingi laki 5 klabu ya Azam FC.

Wambura amesema kamati baada ya kupokea ripoti ya  mechi namba 103 kati ya wenyeji Majimaji FC dhidi ya Azam FC timu ya Azam FC iligoma kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kitndo ambacho ni kosa kwa mujibu wa kanuni za ligi kuu.

Mbali na faini hiyo klabu hiyo pia imetakiwa kuwasilisha ushahidi kuhusu malalamiko yake kwenye mchezo huo ambapo ilidai kutoingia kwenye vyumba hivyo kwasaba vilikuwa vimepuliziwa dawa ambayo ilikuwa inatoa harufu kali.

Kwa upande mwingine mwamuzi wa leo kwenye mechi ya Azam FC dhidi ya Yanga Israel Nkongo ameundiwa kamati ya watu watatu kwaajili ya kuchunguza maamuzi yake kwenye mchezo namba 100 kati ya Tanzania Prisons dhidi ya  Mbeya City kutokana na kuwepo kwa utata katika maamuzi yake.

Azam FC leo itakuwa mwenyeji wa Yanga kwenye mchezo wa ligi kuu raundi ya 15. Hata hivyo Azam FC Jumatatno iliyopita waliwasilisha barua TFF wakiomba kubadilishwa mwamuzi ili achezeshe mwingine badala ya Israel Nkongo lakini ombi lao limetupiliwa mbali.