Jumanne , 24th Nov , 2015

Vinara wa ligi kuu ya Soka Tanzania Bara, Azam FC leo wanatarajiwa kuanza mazoezi kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba SC mwezi ujao.

Benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha Mkuu Stewart Hall, liliwapa mapumziko ya wiki tatu wachezaji mara baada ya kumalizika kwa mechi ya raundi ya tisa ya ligi dhidi ya Toto Africans, iliyoisha kwa Azam FC kushinda mabao 5-0.

Katika taarifa yake, Afisa Habari wa Azam FC, Jaffary Idd, amesema mazoezi hayo yatahusisha wachezaji takribani 10 wa timu kubwa watakaochanganyika na timu ya vijana ya timu hiyo.

Azam FC kwenye mazoezi hayo, itawakosa wachezaji takribani 12 waliokuwa timu za Taifa za Tanzania Bara, Zanzibar, Rwanda, Burundi na Kenya, wakishiriki michuano ya Kombe la Chalenji inayoendelea nchini Ethiopia hadi Desemba 6, mwaka huu.