Aunt Sadaka atoa neno mjadala wa wana Twitter

Jumatano , 3rd Mar , 2021

Mshauri wa malezi, mahusiano na ndoa Aunt Sadaka, amesema kuwa ili kuepusha migogoro kati ya Mama mkwe na mkwewe wa kike ni kuhakikisha kila mtu anaheshimu mipaka yake na kwamba kila mmoja wao anayonafasi kubwa kwa huyo kijana wa kiume.

Mshauri wa malezi, mahusiano na ndoa, Aunt Sadaka

Hayo ameyazungumza hii leo Machi 3, 2021, kufuatia mjadala ulioibuka mitandaoni siku za hivi karibuni ulioonesha misigano inayotokea pale kijana wa kiume anapoamua kuoa na kuanzisha familia huku mama yake mzazi akionesha kuingilia hiyo ndoa ama kutoelewana na mke wa kijana wake.

"Heshima hailazimishwi wewe huna sababu ya kuniheshimu mimi kama sikuheshimu wewe, kila mtu ajue mipaka yake umeolewa kwa mwanangu una mipaka yako kama mtoto na mimi mama nina mipaka yangu kama mama, unajua jambo ambalo tunashindwa kulielewa na kulikubali ni kwamba mimi Mama siwezi kuwa mke kwa mtoto wangu na wewe mke huwezi kuwa Mama kwa mtoto wangu," amesema Aunt Sadaka. 

Aidha Aunt Sadaka ameongeza kuwa "Kila mtu ana nguvu yake, wewe kama mke una nguvu ambayo mimi kama mama siwezi kuwa nayo hata siku moja kwa mtoto wangu na wewe mke huwezi kuwa na nguvu niliyonayo mimi mama kwa mtoto wangu, mimi nitakuheshimu wewe kama mke wa mtoto wangu na wewe ni lazima uniheshimu kwa vitu viwili kwanza nimekuzidi umri na wewe umekuja umeolewa kwangu".