Nikki wa Pili awakingia kifua wafugaji

Wednesday , 11th Jan , 2017

Ikiwa bado migogoro kati ya wakulima na wafugaji inaendelea kushamili nchini msanii wa muziki wa hip hop Nikki wa Pili kutoka Weusi amefunguka na kuweka wazi sababu za migogoro hiyo kushamiri pamoja na kushauri jambo la kufanyika.

Nikki wa Pili

Amesema kuwa mara nyingi wafugaji jamii ya wamasai ambao wanapigana na wakulima katika maeneo mbalimbali nchini ni kutokana na athari za wafugaji hao kuporwa ardhi katika maeneo ya Longido, Serengeti na maeneo mengine.

Nikki wa Pili anadai kutokana na kitendo cha majaji na viongozi mbalimbali kuhodhi maeneo makubwa ya ardhi Morogoro ndiyo kunapelekea vita kubwa kati ya wakulima na wafugaji mkoani humo.

"Wafugaji (wamasai) wanaopigana na wakulima ni waathirika wa kuporwa ardhi, Longido, Serengeti na maeneo mengine, majaji, wanasiasa, wawekezaji wamehodhi ma hekari ya ardhi Morogoro na kuacha vita baina ya wakulima na wafugaji. Wakulima wadogo ni wahanga wa uhodhi wa ardhi wa makampuni ya nje, na wazawa matajiri, majaji, viongozi...ambao wana miliki ma elfu ya hekta za ardhi Morogoro ingawa wengi wanaishi Dar es Salaam" aliandika Nikki wa Pili 

Kutokana na kitendo cha viongozi na watu wenye pesa kuchukua maeneo makubwa makubwa na kuwaacha wanyonge wakiwa na vieneo vidogo ndiyo chanzo cha migogoro hiyo kwa mujibu wa Nikki wa Pili 

"Ardhi imebaki finyu kwa wakulima wadogo na wafugaji, kibaya wanapigana wao na kumuacha adui yao ambao ni waporaji ardhi wa nje na wazawa...chini ya sera za kisasa za kufanya ardhi kuwa bidhaa, haya ni mawazo tu" alisisitiza Nikki wa Pili