Mabibi na mabwana walikuwa wamefurika Car Free Zone katikati ya Mji wa Kigali kutoka huku na kule kwa ajili ya shughuli hiyo, ili kuweza kumuona nguli huyo akiangusha bonge la shoo ambapo ametumbuiza wimbo wake mpya Same Room ambao video yake inazidi kupanda chati mjini Kigali na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Tamasha husika lilikuwa linasubiriwa kwa hamu, hasa kutokana na kwamba wapenzi wa muziki walikuwa wameambiwa kwamba atakuwepo Mani Martin ambaye anakubalika sana nchini Rwanda kwa ngoma za miondoko ya Kiafrika.
Alipopanda jukwaani, mashabiki zake wamempokea kwa nderemo na vifijo kama ishara ya kufurahia ujio wake, na kila wimbo alioimba walikuwa wanaimba naye kwani nyimbo zake wamezikariri.
“Mwaka huu nina malengo ya kuusambaza muziki wangu duniani kote kuanzia Afrika Mashariki, ninafurahi ninapoambiwa na watu kutoka mataifa jirani kuwa wanapenda nyimbo zangu,” Mani Martin amesema.
Katika harakati za kuukuza muziki wake na kuendelea kujizolea umaarufu wa kimataifa, Mani Martin anadai kuwa na mipango ya kufanya kazi na wasanii mbalimbali wa kanda la Afrika Mashariki ambao hakupenda kuwataja kwa majina, akisema “muda si mrefu nitakuambia ni kina nani, ila kwa sasa kuna vitu tunatakiwa tukubaliane kwanza ndipo niweze kubainisha majina yao.”
Baadhi ya mafanikio ya Mani Martin
Nyota njema huonekana alfajiri. Akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 6, ndipo kipaji chake kilipogundulika pale ambapo alikuwa anapenda kuimba darasani na kumvutia mwalimu wake, kwa mujibu wa maelezo yake.
“Mwalimu huyo alinipeleka kanisani ili kuniwezesha kuimarisha kipaji changu cha kuimba. Miaka ilikatika na ilipofika 2005 nikarekodi wimbo wangu wa kwanza Urukumbuzi uliopendwa sana nchini Rwanda na Burundi pia. Nilianza kufanya muziki kama biashara mwaka 2010 ila hapo nilikuwa tayari nimeanza kupokea tuzo tofauti ambazo ndizo zilizonipa motisha.”
Mapema mwaka jana Mani Martin alihudhuria Amani Festival huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kabla hajaachia wimbo aliouita Serafina aliomshirikisha Innoss'b, msanii mkubwa nchini humo.
Miaka 12 baada ya mauaji ya halaiki dhidi ya Watutsi ilimalizika bila hata tuzo moja kutolewa kwa wasanii nchini Rwanda yamkini kwa sababu ilikuwa bado ni kipindi cha simanzi na majonzi.
Mwaka 2006 Mani Martin akawa msanii wa kwanza kutuzwa na kampuni ya Rwanda Music Promotion kwa ushirikiano wa Radio 10 kwa wimbo wake Urukumbuzi aliokuwa akitamba nao enzi hizo kabla hajateuliwa kuliwakilisha taifa lake kwenye PAM Awards mwaka uliofuatia kama msanii bora wa kiume.
Mwaka 2012 kampuni ya Ikirezi Group inayotoa tuzo kwa wasanii bora kila mwaka nchini Rwanda kupitia Salax Awards, ilimkabidhi tuzo ya msanii bora wa ngoma za miondoko ya kiutamaduni (Best Traditional Artist).
Kimataifa, wimbo wake My Destiny ulichaguliwa namba 14 miongoni mwa nyimbo 50 kwenye shindano la BBC World Service. Mwaka wuo huo, Mani Martin aliwakilisha Rwanda kwenye kinyang’anyiro cha mataifa watumiaji wa Kifaransa (Jeux de la Francophonie) ambapo alinyakuwa nishani ya shaba.
Bado tukiendelea kuzungumzia mafanikio ya kijana huyu kutoka nchini Rwanda, ifahamike pia kwamba kipaji chake kilimwezesha kushiriki RFI Discoveries Awards 2013 na kuja kuwa miongoni mwa wasanii kumi bora kwa Afrika Mashariki.
Alipoanza muziki, Mani Martin alikuwa msanii wa nyimbo za injili. Haikupita muda mrefu akaanza kuimba nyimbo za mapenzi na zile za kuhimiza umoja na upendo miongoni mwa Wanyarwanda, ikizingatiwa kuwa Rwanda ilighubikwa na mauaji ya kimbari yaliyosababisha mpasuko mkubwa kwenye jamii.
Ili kuweza kuutazama wimbo huo wa same room bofya hapa https://www.youtube.com/watch?v=3eZvSbc-6jA





