Alhamisi , 15th Feb , 2018

Asilimia kubwa ya vijana au watoto lazima watakuwa wameshaangalia moja au zaidi ya moja ya filamu zake, 'Madea', ambazo huwaacha watazamaji hoi kwa kucheka huku wakiwa na funzo kubwa.

Jina lake halisi ni Emmitt Peery lakini maarufu zaidi kama Tyler au 'Madea', alizaliwa Septemba 13, 1969 huko New Orleans, Louisiana nchini Marekani, akiwa ni miongoni mwa watoto wanne ndani ya familia hiyo.

Tyler Perry aliwahi akisikika akimuelezea baba yake ambaye alikuwa fundi seremala kama baba ambaye jibu lake la kila kitu ni kupiga, alikuwa akiwapiga sana hususan yeye.

Kutokana na hilo Tyler Perry alianza kuhisi huenda sio baba yake, na kumuuliza mama yake kama ni baba yake kweli, mama yake akamjibu ndio baba yake. Mpaka mama yake anafariki alimuuliza tena na kumjibu kuwa ni baba yake, lakini alipofariki aliamua kupima DNA na ndugu yake mmoja, na kugundua kuwa hawakuwa wa baba mmoja.

Licha ya manyanyaso aliyokuwa akimpa, lakini Tyler Perry alisema kuwa hataacha kumjali kama baba yake kwani pamoja na kuwa alikuwa akimnyanyasa, hakuwahi kuwaacha au kuwatelekeza, alihangaika kutafutia chakula na malazi na huduma zingine kama mzazi, hivyo ataendelea kufanya hivyo kama mtoto. Anasema hajui kwa nini mama yake aliamua kumficha ukweli juu ya baba yake halsisi, na iwapo ingewezakana kuzungumza tena na mama yake, hilo ndio lingekuwa swali la kwanza.

Kunyanyaswa kwa Tyler Perry hakukuwa kutoka kwa baba yake tu, bali hata watu wazima wengine ambapo pia aliwahi kusikika akisimulia kwa uchungu kwenye kipindi cha Oprah Winfrey, kuwa alishawahi kutumika kingono na baba wa jirani yake (kumnajisi), vitendo ambavyo vilimfanya Tyler ajaribu hata kujiua akiwa bado mdogo ili kuepukana na maisha hayo.

Akiwa na miaka 16 alibadilisha jina lake na kuwa Tyler kuondokana na jina la baba yake. Alipohitimu elimu ya diploma alifanya kazi mbali mbali bila mafanikio yoyote, mpaka kuja kujigundua ana kipaji gani hasa. Huku akijihusisha na masuala ya kanisa.

Akiwa shabiki mkubwa sana wa kipindi cha Oprah, Tyler alihamasika na kuanza kuandika play mbali mbali ambazo hazikumpa mafanikio, zaidi ya kummalizia visenti alivyokuwa akipata kwenye kazi zake zingine na kufikia hatua ya kukosa pa kuishi, hivyo akawa analala kwenye gari yake ndogo.

Pamoja na hayo yote Tyler Perry hakukata tamaa, aliendelea kuandika play mpaka pale alipoandika play ya 'I have been changed', ambayo ilielezea manyanyaso ya watoto, ubakaji na imani kwa Mungu, na kumpa mafanikio makubwa kwenye ulimwengu wa sanaa na kumfungulia milango zaidi.

Baada ya hapo Tyler Perry aliendelea kuandika play tofauti tofauti na kuzifanyia maonyesho, mpaka pale alipoandika 'Madea' na kuifanyia onyesho, ukawa utambulisho mkubwa kwake kwa dunia nzima mpaka nchi za Afrika kina sisi tukaanza kumjua.

Tyler Perry ameshaandika, kuongoza filamu nyingi zinazohusu maisha ya watu hususan watu weusi, kwa kushirikiana na makampuni makubwa ya utengenezaji wa filamu duniani.

Tyler mpaka sasa ana filamu lukuki alizoandika na kutengeneza yeye, huku akiwachezesha waigizaji mbali zilizotikisa dunia, ikiwemo hiyo Madea, Dady's little girl ambayo alicheza Idris Elba, Why did I get married, For coloured girls, If loving you is wrong na zingine lukuki ambazo ukiangalia lazima zikutoe chozi na kukuachia ujumbe mzito.

Ana utajiri wa dola milioni 600 kwa takwimu zilizotolewa mwaka 2017, ana mtoto mmoja wa kiume anayeitwa Aman, ambaye amezaa na mwanamitindo mwenye asili ya Somalia, Gelila Bekele, ambaye inasemekana amemuoa kwa ndoa ya siri.

 

Tyler Perry kama Madea
Gelila Bekele ambaye ni mke wa Tyler Perry
Emmitt Perry Sr ambaye ni baba wa Tyeler Peryy
Tyler Perry na mama yake mzazi