Jumanne , 17th Nov , 2015

Muigizaji nyota wa filamu ya Two and a Half Men Charlie Sheen, amejitangaza kuwa ni muathirika wa HIV kwenye moja ya vipindi vya televisheni nchini Marekani.

Siku ya Jumatatu wiki hii kituo kimoja cha televisheni nchini humo kilitangaza kuwa muigizaji huyo atatoa tararifa binafsi kwenye kipindi cha siku ya leo na kwanini atasema kuhusu hilo.

“Natakiwa kulimaliza hili ambalo limekuwa na nusu ya ukweli”, alisema Sheen.

Sheen alisema alikutwa na HIV miaka minne iliyopita, na kusisitiza kuwa itakuwa ni vigumu kuwa amemuambukiza mtu mwingine baada ya kugundulika, ingawa anatambua alikuwa amefanya ngono zembe na watu wawili kwa muda huo.

Denise Richards ambaye alikuwa mke wake aligundua ugonjwa wake miaka iliyopita, lakini yeye pamoja na mabinti zake wawili hawajakutwa na maambukizi ya ugonjwa huo aliotambulika nao baada ya wenza hao kutalikiana mwaka 2006.

Muigizaji huyo ambaye aliwahi kutumia madawa ya kulevya, alikiri kuchukua makahaba siku za nyuma, kitendo kilichomfanya afuatiliwe na sheria na mwaka 1998 alipatwa na kiharusi kilichosababishwa na kuzidisha madawa aina ya cocaine.

Sheen mwenye umri wa miaka 50 ni miongoni mwa waigizaji nyota wa Hollywood aliyejipatia umaarufu kwenye filamu ya 'Wall Street” na muendelezo wa filamu ya vichekesho ya Two and a Half Men, ambayo alifukuzwa baada ya kuwa na mgogoro na mtayarishaji wa filamu hiyo.