Msanii Ali Kiba ambaye ameshiriki kama jaji mgeni Dance100%
Akizungumza na EATV Alikiba amesema uwezo uliooneshwa na makundi yaliyoshiriki umemfanya aone kuna sababu ya msingi ya kukuza vipaji vyao kwa kuchukua baadhi ya waliofanya vizuri na kuwajumuisha kwenye kazi zake.
“Nashukuru kwa kuwa Jaji mgeni katika hatua hii ya fainali, jambo ambalo limenifanya nione namna ambavyo kuna vipaji vingi sana katika jamii yetu na kuna baadhi ya vijana nitawachukua kufanya nao kazi katika shughuli zangu za muziki” Amesema Alikiba
Aidha ameupongeza uongozi wa EATV kwa namna ambavyo umebuni namna ya kukuza vipaji vya wasanii kwa kuanzisha shindano la Dance100% maana kuna vipaji vingi sana ambavyo vinavumbuliwa na wengi wanaweza kupata ajira na kutambulika kupitia Dance100%.
Pamoja na hayo Alikiba amewataka washiriki ambao wameshindwa kushika namba moja au mbili wasikate tamaa kwani katika maisha kujituma ni njia ya kupata mafanikio.
Shindano la Dance100% 2016 limefikia hitimisho leo kwa makundi 6 kupambana ambapo kundi la Team Makorokocho limeibuka na ushindi na kujinyakulia kitita cha milioni 7.
Matukio yote ya Dance100% yataoneshwa kupitia kituo cha EATV siku ya Jumapili kuanzia saa moja jioni ambapo shindano limedhaminiwa na Vodacom kwa kushirikiana na Coca- Cola.