Jumamosi , 14th Jul , 2018

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewaagiza viongozi wa mamlaka ya mabonde hapa nchini kuacha kukaa maofisini na badala yake waende kwa wananchi kutoa elimu juu ya kutunza vyanzo vya maji.

Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso

Naibu Waziri huyo ametoa rai hiyo wakati akiwa kwenye eneo la tank la Kazahil Mjini Tabora.

Akiwakumbusha watumishi wa wizara ya maji majukumu yao, Aweso amewataka kuacha tabia ya kutumia lugha mbaya kwa wateja wanaofika katika ofisi zao kutafuta huduma za maji .

Mbali na hayo amewahahakikishia watumishi hao kuwa tayari wizara yake imetenga jumla ya shilingi bilioni 12.29 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji mkoani Tabora hali ambayo itasaidia kuondoa matatizo ya maji Kwa wananchi.

Katika bunge la Bajeti, 2018/19 aliyekuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe (kwa sasa ni waziri wa Ujenzi na Uchukuzi)  aliwasilisha bajeti ya Sh727.35 bilioni ikiwa na ongezeko la zaidi ya Sh79 bilioni ukilingasha na bajeti ya mwaka 2017/18 ya Sh648.01 bilioni.

Kati ya fedha hizo matumizi ya kawaida ni Sh24.4 bilioni ambapo Sh6.7 bilioni sawa asilimia 26 ni kwa ajili ya kugharamia matumizi mengineyo na Sh18.1 bilioni sawa na asilimia 74 ni kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi wa wizara na Chuo cha Maji.