
Mmoja ya mbinu inayohusishwa na imani za kishirikina inayotumiwa na Wananchi wa vijiji Wilayani Mwanga kukabiliana na tembo.
Wakizungumza kwa masikitiko na EATV baadhi ya wakazi na wakulima katika mashamba ya mahindi yaliyovamiwa na tembo, Iddi Kahindu na Paulo Manzi wamesema wameamua kutumia mbinu ya kishirikina ya kuweka dawa ya asili maeneo yanayozunguka mazao ya chakula kuzuia makundi makubwa ya tembo yanayovamia nyakati za usiku na kuharibu mimea.
Wamesema kwa sasa kumekuwepo na changamoto kubwa ya makundi ya tembo kuingia katika mashamba yao na kuharibu mazao ya chakula hali inayohatarisha usalama wa chakula kwa wananchi huku wakilalamikia juu ya ucheleweshaji wa fidia za uharibifu wa mali zao.
Pia wameomgeza kuwa kutokana na athari wanaoiona mbele yao ya tembo hao imefikia wakati ambapo wananchi wamelazimika kutumia imani za kishirikina kutafuta dawa na kuweka pembezoni mwa mashamba yao ili tembo wasikanyange katika mazao yao huku wakiiomba serikali kuhakikisha kuwa tembo wanaoingia katika maeneo ya watu wanaondolewa.
Aidha, kutokana na changamoto za uharibifu wa tembo kwa wananchi, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja, amesema serikali itaongeza askari wa wanyamapori, gari la doria, kupanda miti kuzunguka maeneo ya vijiji vyao pamoja na kuweka mizinga ya nyuki ili kufukuza tembo hao.