Operesheni magari mabovu kuanza kesho

Jumanne , 8th Jun , 2021

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro, ameelekeza Makamanda wa Polisi nchini kufanya operesheni dhidi ya magari mabovu ambayo hayapaswi kuwepo barabarani rasmi kesho, ili kuwahakikishia usalama watumiaji wa vyombo vya moto na kuepuka ajali za barabarani.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro

IGP Sirro amesema hayo leo wakati wa kikao kazi cha kufanya tathmini, mafanikio na changamoto ambapo pia ameelekeza kufanyika kwa operesheni ya mwezi mmoja kwa nchi nzima ili kubaini mianya ya uhalifu na wahalifu.

“Nimeelekeza operesheni ya usalama barabarani, kuna makosa ya barabarani yameanza kujitokeza kama mnavyoona ajali iliyotokea Mbeya, Shinyanga, operesheni dhidi ya magari mabovu nayo itaanza kesho, nawaambia ma RTO, wakuu wa matraffik mikoa yote kufanya operesheni dhidi ya magari mabovu ambayo hayatakiwi kuwepo barabarani” amesema IGP Sirro

Awali akitoa tathimini za operesheni ya wiki moja iliyofanyika jijini Dar es Salaam, IGP Sirro amesema wamefanikiwa kukamata silaha za moto pamoja na wahalifu waliokuwa wakijihusisha katika matukio mbalimbali ya kihalifu.

“Wananchi wa Dar es Salaam wametoa ushirikiano mkubwa sana kwa jeshi la polisi tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, silaha nyingi zimekamatwa wahalifu wengi wamekamatwa, nimeongea na wenyeviti wa mtaa na watendaji Kata wote wa Dar es Salam, tumekuwa na mafanikio makubwa nafikiri wana Dar es Salaam wameona, leo tunahitimisha operesheni lakini tunaanza operesheni nyingine tena ya mwezi mzima na ni nchi nzima” amesema IGP Sirro

Hata hivyo IGP Sirro ameendelea kuwaasa wahalifu waliotoka kutokujihusisha na uhalifu wowote kwani Jeshi la Polisi halitosita kuwachuulia hatua za kisheria mara watapojikita katika kufanya uhalifu.