Jumatatu , 5th Jun , 2023

Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa ofa kwa timu ya Yanga, wachezaji pamoja na viongozi wa klabu hiyo kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti na Hifadhi ya Ngorongoro wakati wa mapumziko yao. 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mohamed Mchengerwa bungeni wakati akiipongeza timu hiyo kwa kuendelea kuitangaza vyema nchi baada ya kushika nafasi ya pili kwenye fainali za Kombe la Shirikisho Barani Afrika sambamba na kutoa mfungaji bora na golikipa bora wa mashindano hayo. 

"Sambamba na hilo niwakaribishe pia mashabiki wote wa Yanga kwenda kujumuika pamoja na wachezaji hao katika safari hiyo katika tarehe itakayotangazwa na utaratibu utakaowekwa, ziara hizo tunapendekeza iitwe, “The CAF Finalists Royal Tour," amesema Waziri Mchengerwa

Aidha Waziri Mchengerwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa kujitoa kwake kupitia  filamu ya The Royal Tour ilivyoleta mafanikio lukuki nchini  si tu watalii kwa kuongezeka, lakini pia nchi  sasa ni kivutio cha mastaa mbalimbali na watu mashuhuri ambao wamekuwa wakija.