Jumamosi , 19th Nov , 2016

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watalaamu wa ujenzi wa mradi wa nyumba za makazi Magomeni watumie utaalamu wao vizuri na wakamilishe kwa wakati.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo wakati alipokagua ujenzi wa nyumba hizo zinazojengwa na wataalamu kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) eneo la Magomeni Kota jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amewataka wataalamu hao waendelee kufanya kazi hiyo kwa kufuata misingi ya weledi wa taalauma yao kwani Serikali inawaamini., na kwamba wamepewa dhamana hiyo kubwa ya kukamilisha ujenzi huo ili wananchi waliokuwa wanaishi hapo waweze kurudi katika makazi yao,

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ushauri wa TBA, Mhandisi Edwin Nnunduma amesema awamu ya kwanza ya ujenzi huo itahusisha majengo matano ya makazi, ambapo kati ya majengo hayo matano, manne yatakuwa na ghorofa nane na moja litakuwa na ghorofa tisa, ambapo wakazi zaidi ya 600 waliokuwa wanaishi eneo hilo tangu zamani watakabidhiwa,

Mhandisi Nnunduma amesema majengo hayo yanajengwa kwa teknolojia ambayo imezingatia uwezo wa wakazi wake ambapo ina majiko yanayoweza kutumia kuni na mkaa.

Amesema mradi huo ambao unajengwa kwa awamu tofauti utahusisha ujenzi wa nyumba za makazi, maduka makubwa na ya kisasa pamoja na ofisi.

Mhandisi huyo amesema awamu ya kwanza iliyoanza Oktoba Mosi, mwaka huu inahusisha ujenzi wa nyumba za makazi ya wananchi waliokuwa wanaishi katika eneo hilo ambayo inatarajiwa kukamilika Oktoba, mwakani.