Alhamisi , 29th Sep , 2016

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa amewataka madiwani kuwa waadilifu na waminifu katika kutekeleza majukumu yao mbalimbali ikiwemo kusimamia miradi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi.

Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Kasim Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema hayo wakati akiongea na madiwani katika wilaya mpya ya Kibiti kwenye ziara yake ya kikazi Mkoani Pwani ambapo amesema wananchi wanategemea maendeleo yao kutokana na miradi mbalimbali inayosimamiwa na madiwani hao.

Waziri Majaliwa amesema serikali ya awamu ya tano haitamvumilia diwani yeyote atakayebainika kutumia miradi ya maendeleo kujinufaisha mwenyewe lakini pamoja na kuingia mikataba hewa ambayo inalitia taifa hasara.

Katika hatua nyingine akiongea na wakazi wa eneo la Bungu ambao walisimamisha msafara wake kwa madai ya kutolipwa fidia sehemu zao ulipopita mradi wa umeme wa REA aliwahakikisha kulipwa fidia hiyo.

Aidha Waziri Majaliwa ameongeza kuwa serikali itahakikisha kila kijiji kinapata umeme kwenye mradi wa REA awamu ya tatu kwa hiyo vijiji vilivyokosa umeme wakazi wake wasivunjike moyo kwa sababu serikali inafanya kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wote.