
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Waziri Majaliwa ameyasema hayo leo Julai 17, 2022, wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua daraja hilo lililojengwa kwa kutumia teknolojia rahisi ya mawe akiwa kwenye ziara yake mkoani Singida, daraja hilo limegharimu shilingi milioni 102.
"Nawapongeza wahandisi wa mkoa wa Singida kwa ubunifu huu wa ujenzi wa daraja hili la mawe mlilolijenga kwa ubora na kwa gharama nafuu," amesema Waziri Mkuu
"Daraja hili hapa miaka yote tulishindwa kulijenga kwa sababu ya gharama, ilikuwa lazima tupate shilingi milioni 500 kumbe Mainjinia wetu kwa utalaam wao wana uwezo wa kujenga daraja la kudumu na kwa gharama nafuu, kupitia vikao vyenu vya TARURA hii taaluma muifikishe kwa wahandisi wengine ili kila mmoja kwenye mkoa wake aitumie na kwa mtindo huu tutajenga madaraja kwa gharama nafuu," ameongeza Waziri Mkuu
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) mkoa wa Singida Mhandisi David Tembo, amesema ujenzi wa daraja hilo ni sehemu ya kazi zilizofanyika katika mkataba wa matengenezo ya muda maalumu ya barabara ya Mwando-Miganga-Kinandili yenye urefu wa kilomita 12.39, kazi zote zimegharimu kiasi cha fedha shilingi milioni 444.