Jumatatu , 13th Sep , 2021

Waziri wa Maji Jumaa Aweso, ametoa muda wa miezi mitatu kwa watalaam wa maji kutoka wizarani na wahandisi wa maji wilayani Karagwe mkoani Kagera kuhakikisha miradi yote ambayo imekamilika lakini haitoi maji, inakamilika ndani ya kipindi hicho na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Waziri wa Maji Jumaa Aweso

Akizungumza baada ya kutembelea chanzo cha maji cha Omururongo kilichoko wilayani humo, Waziri Aweso, amesema kuwa timu ya wataalamu kutoka wizarani inapaswa kuwasili Jumatatu ya leo katika wilaya ya Karagwe, na kuanza kushughulikia tatizo hilo.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara mbele ya Waziri huyo, baadhi ya wakazi wa miji ya Kayanga na Omurushaka, iliyoko wilayani humo wamesema kuwa wanakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji, hali inayosababisha kununua ndoo moja ya maji yenye ujazo wa lita 20 kwa kati ya shilingi 500 hadi 1,000 kutoka katika visima vya watu binafsi.