Jumamosi , 12th Nov , 2016

Wauguzi nchini wametakiwa kujiunga katika vyama vya akiba na kukopa (SACCOS) ili iwe njia ya kujikwamua na changamoto za maisha.

Rai hiyo imetolewa leo Jijini Dar es salaam na Afisa ushirika wa Manispaa ya Kinondoni Rosemery Mkosamali, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Pili wa Saccos ya wauguzi nchini, inayoitwa Tann Saccos.

Bi. Mkosamali amesema njia pekee ya wauguzi katika kujikwamua na hali ngumu ni kujiunga katika Saccos, ili iweze kuwasaidia katika kukopa ambayo na kuanzisha biashara mbali mbali, ambazo zitasaidia kutatua tatizo la ugumu wa maisha.

“Kuungana na kuanzisha Saccos kama hii itawasaidieni katika kujikwamua kwa kujipatia kipato, mtakavyokopeshana fedha hizo zitasaidia katika kutatua matatizo yenu", liesema Bi Mkosamali

Hata hivyo Bi. Mkosamali ambaye kitaaluma ni mchumi, amesema kitendo cha wauguzi hao kuungana na kufungua Saccos hiyo kitaweza kukuza uchumi wa nchi huku akizitaka jamii kuiga mfano kwa wauguzi hao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Saccos hiyo, Adam Francis amesema kwa sasa wana wanachama 365 ambao ni wauguzi walioajiriwa katika idara za Afya nchini, na kwa sasa wataanza rasmi kuwakopesha wauguzi hao, kwani wana mtaji unaofikia milioni 12, na wanatarajia kupata faida ya zaidi ya milioni 10 zitazotokana na riba kutokana na mikopo watakao toa kwa wauguzi hao.

Hata hivyo, amebainisha kuwa mikopo hiyo ikayotolewa itakuwa na riba ndogo ambayo inamuwezesha muuguzi kukopa na kurejesha, huku akiwataka wauguzi wengine kujiunga na Saccos hiyo kama lengo la kujipatia kipato.