
Akiwaongoza wakazi wa Arusha kuomboleza msiba katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid, Makamu wa Rais, Mh. Samia Suluhu amesema kwamba Madaktari hao walikuwa watalii na gari lao lilikuwa mbele ya 'bus' la wanafunzi na hata baada ya ajali kutokea wao ndio walikuwa watu wa kwanza kutoa msaada wa kitaalamu.
Katika hotuba yake Makamu wa rais amesema kuwa hata baada ya kutoa msaada watalii hao kutoka shirika la afya nchini Marekani wameahidi kujitolea kuwapatia matibabu wanafunzi watatu ambao ni majeruhi wa ajali hiyo na hata msaada kutoka nje ya nchi wapo tayari kututoa.
Aidha, Mh. Samia ameongeza kwamba ajali hiyo ya Mkoa wa Arusha imewafumbua macho serikali kufanya marekebisho mbalimbali ili kuepuka ajali, huku akifafanua serikali itahakikisha inaboresha alama za barabarani na kuimarisha ulinzi na usalama.
"Serikali inapambana sana na matumizi ya dawa za kulevya, na vyanzo vingi vya ajali vinasababishwa na matumizi ya vilevi kwa madereva naomba niwaombe sana madereva muwe waadailifu. Hata hivyo madereva ni wajibu wenu kuhakikisha mnabeba abiria kulingana na uwezo uliowekwa. haipendezi nchi yetu ajali kutokea kila siku. Kwa upande wetu serikali niwaahidi tutahakikisha tunaboresha miundombinu, alama za barabarani pamoja na usalama wa barabarani ili kukabiliana na ajali hizi" - Mh. Samia Suluhu.
Pamoja na hayo Mh. Samia amewafariji wafiwa kwa kutaka wafahamu msiba wa wanafunzi, walimu pamoja na dereva wa Lucky Vicent ni wa Taifa zima, huku akiwasisitiza watu kuwa waangalifu barabarani kwani matokeo ya ajali huwa ni misiba mikubwa kama huu wa leo.